Jiografia na tabianchi ya Uswidi

Sveriges geografi och klimat – swahili

Katika ukurasa huu unaweza kusoma kuhusu jinsi Uswidi ilivyogawanywa kijiografia, kuhusu tabianchi na misimu tofauti.

Muhtasari

  • Wakimbizi waliohamia nchini wanapewa makazi mapya kote nchini Uswidi.
  • Uswidi imegawanywa katika kaunti zilizogawanywa katika sehemu tatu, Norrland, Svealand na Götaland. Hali na tabianchi hutofautiana kati ya kaunti tofauti.
  • Uswidi ina misimu minne tofauti na hali ya hewa hutofautiana kati ya misimu.
  • Unahitaji kuwa na nguo zinazofaa hali tofauti ya hewa na misimu. Kwa mfano, katika majira ya baridi unahitaji mavazi yenye joto ukiwa nje.

Ukweli kuhusu Uswidi

Uswidi iko kaskazini mwa Ulaya. Ni mojawapo ya nchi kubwa zaidi barani Ulaya, lakini ina wakazi wapatao milioni kumi. Nchi hii ina urefu wa kilomita 1,600 na upana wa kilomita 500. Jiji mkuu ni Stockholm na lugha rasmi ni Kiswidi.

Uswidi iko kwenye Bahari ya Baltic na ina ukanda wake wa pwani. Nchi jirani za Uswidi ni Norwei upande wa magharibi, Denmark upande wa kusini na Ufini upande wa mashariki. Upande wa mashariki, Uswidi inapakana na Bahari ya Baltic kwa urefu wote wa nchi. Uswidi ina uhusiano mzuri na nchi jirani.

Nafasi ya Uswidi ulimwenguni.

Nafasi ya Uswidi ulimwenguni. Michoro: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Elin Hägg

Tofauti za kikanda

Uswidi imegawanywa katika sehemu tatu za nchi, na mazingira ya asili na tabianchi hutofautiana ndani na kati ya sehemu hizi tatu za nchi. Kuna miji na vijiji katika sehemu zote za Uswidi, lakini Uswidi ya kusini na kati ina wakazi wengi na miji mikubwa zaidi.

  • Norrland (kaskazini mwa Uswidi) ina milima, misitu na bahari nyingi. Hakuna ardhi kubwa ya kilimo na wakazi ni wachache kuliko sehemu iliyosalia ya nchi. Uswidi ya Kaskazini inajulikana kwa mazingira ya asili ya kupendeza.
  • Svealand (Uswidi ya kati) pia ina misitu mingi lakini pia ardhi zaidi ya kilimo. Jiji kuu la Uswidi, Stockholm, liko katikati mwa Uswidi kwenye upande wa mashariki.
  • Götaland (kusini mwa Uswidi) ina mashamba mengi na fukwe ndefu. Miji mikubwa ya Gothenburg na Malmö iko kusini mwa Uswidi.

Wakimbizi wanaohamia nchini wanapewa makazi mapya kwenye manispaa katika sehemu zote za Uswidi. Bila kujali iwapo unaishi mjini au mashambani, kila mtu nchini Uswidi anaweza kufikia elimu na huduma nyingine, kama vile huduma ya afya na utunzaji wa watoto.

Karta: Mikoa ya Uswidi ya Norrland, Svealand na Götaland.

Sehemu tatu za Uswidi: Norrland, Svealand na Götaland. Michoro: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Elin Hägg

Hali ya hewa na tabianchi

Uswidi ina misimu minne na hali tofauti ya hewa, lakini kina msimu una mvua na jua. Tofauti kati ya misimu inaonekana zaidi katika hali-joto, mimea na muda wa mwanga mchana kutwa.

Katika sehemu za kaskazini, hali ya hewa na baridi kuliko sehemu za kusini. Huko, majira ya baridi ni ndefu na kuna theluji nyingi zaidi, lakini majira ya kiangazi ni joto nchini kote. Eneo la kaskazini mwa Uswidi kwenye ramani ya dunia linaonyesha kwamba nchi ina saa nyingi za jua wakati wa majira ya joto na chache katika majira ya baridi.

Tofauti hizi zinaonekana hasa kaskazini mwa Uswidi, ambapo kuna mwangaza karibu saa 24 kwa siku wakati wa majira ya kiangazi na giza katika saa nyingi za siku wakati wa majira ya baridi.

Majira ya Baridi

Desemba, Januari na Februari.

Vinter med snöplog på väg.

Majira ya baridi ni wakati wa baridi zaidi wa mwaka. Hali-joto hupungua na mara nyingi ni nyuzi chini ya sifuri. Theluji hunyesha, hasa kaskazini mwa nchi na theluji hubaki ardhini kwa muda mrefu. Maziwa na maji mengine yanaweza kuganda na kuwa barafu. Wakazi nao huenda shuleni na kufanya kazi kama kawaida hata wakati kuna baridi na theluji. Theluji nyingi huondolewa mitaani na barabarani. Badala ya theluji kunaweza kuwa na mvua wakati wa majira ya baridi, hasa kusini mwa Uswidi.

Kuna shughuli nyingi za nje na michezo ya majira ya baridi, kama vile kuteleza, kuteleza barafuni na kuskii. Shuleni na katika shule ya chekechea, watoto huwa nje bila kujali hali ya hewa na wakati wa mwaka. Nguo za joto hulinda mwili dhidi ya baridi. Kwa sababu ya hali ya hewa ya baridi, watu wengi huwa ndani ya nyumba kuliko katika misimu mingine. Ndani ya nyumba ni joto hata wakati wa baridi kwa sababu nyumba zinazuia baridi na zina mifumo mizuri ya kupasha joto.

Ni muhimu kuvaa mavazi yenye joto na kuvaa nguo nyingi ukiwa nje wakati wa majira ya baridi, ili kulinda mwili mzima. Kutovaa mavazi yenye joto kwa muda mrefu wakati wa baridi kunaweza kuwa na madhara kwenye mwili.

Hivi ndivyo unavyoweza kuvaa:

  • Jaketi yenye joto na ovaroli zenye joto kwa watoto.
  • Kofia yenye joto kichwani.
  • Glavu mkononi.
  • Shali au skafu.
  • Viatu vyenye joto na soksi.

Majira ya Kuchipua

Machi, Aprili na Mei.

Majira ya kuchipua ni wakati wa mpito ambapo majira ya baridi inabadilika kuwa majira ya joto. Wakati wa majira ya kuchipua , hali-joto huongezeka, theluji na barafu huanza kuyeyuka na mimea inaanza kubadilika kuwa rangi ya kijani. Siku zinaanza kung'aa na kuwa ndefu.

Jaketi au koti, shali, glavu na viatu visivyopenyeza maji mara nyingi huhitajika nje.

Majira ya Joto

Juni, Julai na Agosti.

Familia ufukweni wakati wa majira ya joto.

Picha: Anna Hållams/imagebank.sweden.se

Majira ya joto ni msimu wa joto jingi zaidi wa mwaka. Hali ya hewa mara nyingi ni ya joto na kuna jua, mazingira ya asili ni ya kijani na mimea inachanua. Siku nyingine zinaweza kuwa na mvua, mawingu na baridi. Siku ni ndefu na jioni ni angavu.

Katika majira ya joto watu wengi hujishughulisha na shughuli za nje au kuchangamana katika bustani na sehemu za kuoga na kufurahia hali ya hewa na jua.

Kwa kawaida nguo nyembamba zinatosha mchana kutwa na kwa kawaida huhitaji kutumia jaketi.

Majira ya Kupukutika kwa Majani

Septemba, Oktoba na Novemba.

Watoto anacheza kwenye mvua ya majira ya kupukutika kwa majani.

Picha: Emelie Asplund/imagebank.sweden.se

Majira ya kupukutika kwa majani ni wakati wa mpito ambapo majira ya joto inabadilika kuwa majira ya baridi. Hali ya hewa inazidi kuwa baridi, mimea inanyauka na majani inaanguka kutoka kwenye miti. Siku zinazidi kuwa fupi na giza tena. Wakati mwingine kuna mawingu na mvua. Mwishoni mwa majira ya kupukutika kwa majani, mvua ya theluji inaweza kuanza, hasa katika sehemu za kaskazini mwa nchi. Katika sehemu za kaskazini mwa nchi, theluji huyeyuka haraka.

Ni vizuri kuwa na jaketi au koti, shali, glavu na viatu visivyopenyeza maji ukiwa nje. Lakini si lazima uvae mavazi yako ya nje yenye joto zaidi.

Maswali ya kufikiria

  • Je, kuna misimu mingapi katika nchi yako ya asili?
  • Je, una nguo zenye joto unazoweza kubeba ukija Uswidi?

Last updated: